Tanzania and Zanzibar culture, life and travel online
Follow Us oin our Facebook Group RSS Feed

Z-a-n-z-i-b-a-r by Dismas Sekibaha

Zawadi iliyofichika,
Amana ya Uhakika,
Nuru iliyoumbika,
Zamani ilisifika,
Imara yatambulika,
Bandari ya kukumbuka,
Ambatana nami,
Rejea,

Zawadi yetu,
Asubuhi na usiku nuru yetu,
Nakshi maishani mwetu,
Zamaradi machoni mwa watu,
Inapendeza rangi za chatu,
Bahati ya utatu,
Ambatana nami,
Rejea,

Zabibu yakubalika,
Amani iliyotukuka,
Nishati kwa waliopotoka,
Zaidi ya moto kwenye ukoka,
Inastahili kuheshimika,
Bustani ya waliopevuka,
Ambatana nami,
Rejea,

Zamaradi utamu wake,
Asali maisha yake,
Neema kwa watu wake,
Ziada yake,
Inawajali wanawake,
Biriani chakula chake,
Ambatana nami,
Rejea

Zaidi na zaidi,
Almasi isiyo na kodi,
Ngoma isiyo na makuadi,
Zumari lipigalo hodi,
Itikia kwa juhudi,
Bohari la wenye midadi,
Ambatana nami,
Rejea,

Zamiminika Neema,
Amali itunzayo chema,
Neema zenye rehema,
Zafananishwa na pema,
Imulikayo mema,
Baragumu, chuki linazima,
Ambatana nami,
Rejea,

Zitazame pembe zake,
Angalia anga lake,
Nakshi na nyumba zake,
Zingatia muono wake,
Imba nyimbo zake,
Bahati kuishi kwake,
Ambatana nami,
Rejea,

Zamia majini,
Angalia mitini,
Ndege angani,
Zikri mitaani,
Imani maishani,
Bahati ya ukweni,
Ambatana nami,
Rejea,

Zingatia yaliyo ndani,
Asili ya burudani,
Ndimi, lafudhi laini,
Zenye heshima mitaani,
Ingia melkebuni,
Burudika pamoja nami,
Ambatana nami,
Rejea,

Zama za kale mpaka leo,
Aghalabu kuona vileo,
Ndiyo sababu likawa kimbilio,
Zaidi ya mawio na machweo,
Ibada zikawa pembejeo,
Baba wa misingi ya leo,
Ambatana nami,
Rejea,

Zawadi hii ni mali,
Angalia wakati wa futari,
Ndugu na watu wa serikali,
Zinduko la wenye heri,
Ingia umuone mwari,
Burudika usikae mbali,
Ambatana nami,
Rejea,

Zitokapo salamu za kheri,
Asalaam Aleikum ni johari,
Nahau za kiswahili,
Zasafiri nchi za mbali,
Ingia uone fahari,
Burudika usilete shari,
Ambatana nami,
Rejea.